Wagombea watano wa tuzo ya BBC kwa
mwanasoka bora wa mwaka 2015 wametangazwa kwenye hafla maalum
iliyoandaliwa mjini Johannesburg, Afrika Kusini.
Mshindi ataamuliwa na mashabiki wa soka Afrika ambao watapewa fursa kupiga kura hadi tarehe 30, Novemba.
Unaweza kupiga kura kwa kutuma ujumbe mfupi wa simu kwa nambari +44 7786 20 20 08:
- Ujumbe 1 kwa-Emerick Aubameyang
- Ujumbe 2 kwa André Ayew
- Ujumbe 3 kwa Yacine Brahimi
- Ujumbe 4 kwa Sadio Mané
- Ujumbe 5 kwa Yaya Touré
Wagombea wa tatu mwaka huu waliopigiwa kura na wanahabari 46 kutoka Afrika wamewahi kushinda tuzo hiyo: Ayew (2011), Touré (2013) na Brahimi (2014).
WASIFU WA AUBAMEYANG;
Mshambuliaji wa Gabon na Borussia
Dortmund Pierre-Emerick Aubameyang amekuwa na mwaka wenye mafanikio,
akiwa amefunga magoli mengi na kuweka rekodi mpya ya ufungaji Ujerumani.
Lakini Mgabon huyu alifanya hivyo, akifunga katika mechi nane za mwanzo za ligi za msimu. Akiipita rekodi ya awali kwa michezo miwili.
Alipofunga katika mechi ambayo walicharazwa 5-1 na Bayern Munich mwanzoni mwa mwezi Oktoba, kijana huyo mwenye miaka 26 aliingia katika vitabu vya kumbukumbu kwa sababu nyingine.
Kwa kuwa alikuwa amefunga katika mechi mbili za mwisho za mwaka 2014-15, alikuwa pia amefunga mabao mfululizo katika mechi 10 za Bundesliga ikiwa ni rekodi ambayo mtu pekee aliyekuwa ameifikia ni Klaus Allofs miaka 30 iliyopita.
“Babangu (mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Gabon) aliniambia kuwa unaweza kufunga katika kila mechi ukitaka,” Aubameyang aliiambia BBC Sport.
“Lakini unahitaji umakini wa hali ya juu kabisa na hilo ndilo ninalolifanyia kazi.”
Baada ya mechi moja ambayo hakufunga (ingawa alitoa usaidizi mara mbili) Mgabon huyu wa kwanza kucheza katika ligi kuu ya Ujerumani alifanya mambo kupitia kile yeye mwenyewe anachokiita...tukio muhimu zaidi kwake mwaka huu.
Katika mechi mbili zilizofuata katika Bundesliga na Europa League alifunga mabao matatu matatu yaani hat-tricks mfululizo.
Baada ya kuongeza ufasaha wa kufunga kwenye kasi yake, ‘Auba’ alifunga mabao 20 katika mechi 17 za kwanza alizochezea Dortmund msimu 2015-16.
Msimu wa 2014-15 Dortmund walimaliza katika nafasi ya 7 baada ya mwanzo mbaya lakini Aubameyang ndiye aliyeng’aa zaidi. Winga huyo aliyebadilika kuwa mshambuliaji alimaliza akiwa kuwa mfungaji bora wa klabu hiyo akiwa na magoli 16 ya ligi.
Pia alifunga matano katika DFB Pokal msimu uliopita, ikiwemo katika robo fainali, nusu fainali dhidi ya Bayern na fainali yenyewe waliposhindwa na Wolfsburg.
Kwa hivyo haikuwa ajabu pale Dortmund waliposema kwamba Aubameyang, waliyemnunua kutoka St Etienne ya Ufaransa 2013, alikuwa akimezewa mate na klabu kadha kuu za Ulaya
Ingawa kiwango chake cha uchezaji akichezea klabu kimevutia sana, Aubameyang bila shaka hawezi akataka kukumbuka fainali za Kombe la Taifa Bingwa Afrika kwani hawakufana. Hata hivyo alifunga moja kati ya magoli mawili yaliyofungwa na Gabon dimba hilo nchini Equatorial Guinea.
Aubameyang, mchezaji wa zamani wa timu ya vijana ya Milan na timu ya vijana ya Ufaransa, ameingia katika orodha ya wanaowania tuzo ya mwanakandanda bora wa mwaka wa BBC kwa mwaka wa tatu mtawalia.
WASIFU WA ANDRE AYEW;
Wengi wamekuwa wakizungumzia ugumu
wa kuzoea ligi kuu ya England, lakini Mghana André Ayew alifanya hilo
likose maana baada ya kutua kwa kishindo Swansea.
Bao la pili lilifuata akicheza mechi yake ya kwanza uwanja wa nyumbani, lakini ni ushindi wa 2-1 dhidi ya timu ya Manchester United mwishoni mwa mwezi Agosti uliotangaza kufika kwa Ayew.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 alisawazishia timu yake iliyokuwa imelezwa, kabla ya kusaidia kuunda bao la ushindi la Bafetimbi Gomis, kwa pasi safi kwa kutumia kisigino.
Muda si muda, mchezaji huyo ambaye alizaliwa na sifa za kiongozi alitawazwa mchezaji bora Ligi ya Premia wa mwezi Agosti na kusifiwa kama mojawapo ya nyota wazuri walionunuliwa msimu huu.
Ni jambo la kushangaza ikizingatiwa kwamba Swansea walikuwa wamesajili akiwa hana klabu yoyote.
Ayew, ambaye ni mtoto wa nguli wa mpira ulimwenguni Abedi 'Pele', Ayew, ana ustadi, uthabiti na ujanja mchezoni. Ni kana kwamba amefika nyumbani katika ligi aliyoitamani sana.
“Huu ulikuwa ndio wakati mwafaka kwangu kucheza katika Ligi ya Premia na kutimiza ndoto yangu,” aliambia BBC Sport.
“Nilizoea uchezaji wa hapa vyema kwa sababu niliingia mapema. Nilikuwa na mufa wa kujiandaa kipindi chote cha kabla ya msimu, nilifahamiana na wachezaji wenzangu, na wakanipa ujasiri na uwajibikaji.”
Na amejibu kwa kufunga mabao MATANO na kusaidia ufungaji wa bao MOJA katika mechi KUMI NA MOJA za kwanza alizocheza Ligi ya Premia.
Kuwasili kwake UIngereza kulitokea baada yake kuwa na msimu mbaya na Marseille, waliomaliza nafasi ya nne katika ligi kuu ya Ufaransa na kuondolewa kutoka mashindano mawili ya vikombe mapema.
Lakini Ayew, alifana bado, ustadi wake ukifanya asifiwe sana alipokuwa akiondoka katika klabu hiyo aliyojiunga nayo kama kijana baada ya kukaa miaka 11 na kushinda vikombe viwili vya ligi (na kufunga mabao 61).
Wakati alipokuwa akiwapa mkono wa kwaheri mashabiki wa Velodrome mnamo mwezi Mai, Ayew, aliyekata kipande cha zulia akahifadhi kama kumbukumbu, alishindwa kuzuia machozi pale mashabiki walipokuwa wakiliimba jina lake.
Na hiyo haikuwa mara yake ya kwanza kutokwa na machozi mwaka huu.
Mwezi Februari, alilia baada ya Ghana kukosa fursa ya kushinda Kombe la Taifa Bingwa Afrika mara ya kwanza katika miaka 33 waliposhindwa na Ivory Coast kupitia mikwaju ya penalti.
Ayew alifunga mkwaju wake na naibu nahodha huyu wa timu ya Ghana pia alimaliza kama mfungaji mabao bora, akishikilia nafasi hiyo pamoja na wachezaji wengine watano waliofunga mabao matatu.
Muhimu zaidi lilikuwa bao lake la ushindi la dakika ya 83 dhidi ya Afrika Kusini, mechi iliyokuwa ya mwisho kwa Black Stars kundini, iliyohakikisha wanamaliza kileleni katika kundi lao.
Alishinda tuzo ya BBC ya mwanakandanda bora wa Afrika wa mwaka 2011 lakini je, Ayew anaweza kuwa Mghana wa kwanza kushinda tuzo hii mara mbili?
WASIFU WA SADIO MANE;
Sadio Mane huenda hakushinda
chochote mwaka wa 2015 lakini wakati mshambuliaji huyo wa kilabu ya
Southampton alipofunga mabao matatu pekee yake, ndani ya sekunde 176
katika ushindi wa nyumbani wa 6-1 dhidi ya Aston Villa mnamo mwezi
Aprili ,alivunja rekodi ya ligi ya Uingereza ambayo huenda ikakaa kwa
mda mrefu.
Mabao hayo yaliwavutia wengi ulimwenguni na hivyobasi kumuorodhesha mchezaji huyo wa Senegal ambaye amekuwa mshambuliaji hatari zaidi latika ligi ya Uingereza.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 aliweka rekodi nzuri ya ufungaji mabao tangu alipowasili katika kilabu hiyo ya St Marys kwa kitita cha dola milioni 12 mnamo mwezi Septemba mwaka 2014 kutoka kilabu ya Red Bull Salzburg,ambapo alikuwa ameshinda ubingwa wa ligi na makombe mawili ya ligi hiyo.
Lakini kwa kuwa umaarufu wa ligi ya Austria uko chini mara mbili ya ule wa ligi ya Uingereza,umahiri wake ulitiliwa shaka.
Huku mabao hayo matatu yakivutia vichwa vya habari,ikiwemo uchezaji wake mzuri aliouonyesha dhidi ya Chelsea mnamo mwezi Octoba,ambapo alifunga bao moja na kusababisha jingine katika ushindi wa mabao 3-1, umuhimu wake sasa umebainika.
Mane ambaye anaweza kucheza mahala popote katika safu ya mashambulizi,ikiwemo katika wingi,katikati na mbele iwapo atahitajika,alikuwa mchezaji bora baada ya kuchangia katika kuishinda timu ya Jose Mourinho ambayo ilikuwa inapoteza kwa mara ya saba nyumbani akiwa mkufunzi wake.
Bao lake la kusawazisha dhidi ya Liverpool,ni miongoni mwa mabao matatu ambayo Mane amefunga katika mechi 11 za ligi ya Uingereza lakini pia likiwa miongoni mwa pasi nne.
Amejiimarisha katika kampeni yake ya ligi ya Uingereza,baada kutoa pasi moja baada ya kipindi cha Krisimasi alipofunga mabao 9 kati ya mechi 19.
Mabao 10 aliyofunga yalijumlisha 1/5 ya mabao yote yaliofungwa na Southampton na kuisaidia kilabu hiyo kufuzu katika ligi ya Ulaya kwa mara ya pili tangu mwaka 1980.
Akiwa mwepesi na mwenye kasi ,pamoja na ujuzi wa kutamba na mpira mchezaji huyo alianza kuhusishwa na uhamisho wa kuelekea kilabu ya Manchester United ,licha ya Southampton kukana kupata ombi lolote kutoka kwa mabingwa hao wa zamani wa ligi ya klabu bingwa Ulaya.
Mchezo wake mzuri umemfanya Mane kuorodheshwa miongoni mwa wachezaji wanaowania taji la kila mwaka la BBC barani Afrika kwa mara ya kwanza, akilazimika kusahau yale yaliotokea katika michuano ya Afrika mwaka 2015.
Baada ya kupata jeraha siku 16 kabla ya michuano ya kombe hilo kuanza,ilidhaniwa Mane hatoshiriki katika mashindano hayo ,lakini licha ya kuorodheshwa katika mechi mbili za mwisho hakuweza kuisadia Senegal ambayo iliondolewa katika awamu ya makundi.
WASIFU WA BRAHIMI;
Bingwa mtetezi wa tuzo ya Mwanasoka
bora wa Mwaka, Yacine Brahimi anapigania kuwa mchezaji wa pili kuhifadi
tuzo yake, baada ya Mnigeria Jay Jay Okocha kufanya hivyo kwa kushinda
2003 na 2004.
“Ninazidi kupata uzoefu kwa kucheza dhidi ya timu kubwa,” mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 25 aliambia BBC Sport. “Hii ina maana unajifunza zaidi unafanya kazi kwa bidii kila siku ili uwe bora.”
Ni lazima anajiandaa.
Moja kati ya mafanikio makubwa aliyoyapata ilikuwa mwaka 2014/15 katika harakati za kusaka ubingwa wa klabu Bigwa barani Ulaya alipogaragaza mpira mara 42 na ambapo waliomzidi pekee ni mchezaji wa Barcelona Lionel Messi na Eden Hazard wa Chelsea.
Magoli yake matano yaliisaida Porto kufikia robo fainali ya Klabu Bigwa barani Ulaya kwa mara ya kwanza baada ya miaka sita.
Na kwa kufufua kumbukumbu ya mwaka 1987 walipofikia fainali ya Kombe la Ulaya dhidi ya Bayern Munich, Wareno hao waliandika rekodi nyingine kwa kuwabwaga Wajeruman hao waliposhinda mkondo wa kwanza katika robo fainali kwa jumla ya magoli 3 -1.
Hata hivyo, walishindwa baada ya kufungwa 6-1 mechi ya marudiano.
Hilo lilikuwa jambo la kukumbukwa katika msimu ambao Porto walimaliza ligi wakiwa nambari mbili, huku Brahimi akifunga magoli saba katika ligi ya Ureno Primeira Liga, na kufikisha jumla ya mabao 13 maisha yake ya uchezaji.
Baada ya kumalizika kwa msimu wa ligi Porto ilimmulika mwanasoka huyo aliyewahi kuchezea Ufaransa katika michuano vijana ya kimataifa na kuongeza hadhi yake kwa kuongeza kifungu cha kumnunua kutoka euro milioni 50 hadi milioni 60.
Ingawa mchezaji huyu mwenye kasi sana hajafikia mabao aliyoyafunga mwaka jana, ameendelea kung’aa 2015-16 akipokezwa tuzo kadha kama mchezaji bora wa mechi.
Moja kati za hizo ilikuwa ni Septemba katika mechi ya Klabu Bigwa Ulaya wakati Porto ilipoumana na Chelsea na akachangia katika ufungaji wa magoli yote mawili mechi hiyo waliyoshinda nyumbani (Porto walishinda mechi zao 19 za kwanza nyumbani 2015).
Mchezaji huyo aliyetoka akademi inayoheshimika sana Ufaransa ya Clairefontaine tayari ameshapachika magoli saba katika mechi kumi na nne za kwanza alizocheza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya
Akiwa kivutio kwa wengi Brahimi anajitahidi kuifanya Porto iwe na mafanikio kama wachezaji waliomtangulia James Rodriguez, Hulk na Falcao katika moja klabu kubwa katika siku za hivi karibuni.
Kwa uwezo wake wa kugeuka kwa wepesi kumiliki mpira na ufundi wa hali ya juu Brahimi amekuwa akisumbua ngome za wapinzani.
“Sifahamu wachezaji wengi wanaoweza kufanya anachokifanya,” Kocha wa Algeria Christian Gourcuff amesema mwaka huu.
Tishio la mchezaji huyo limedhihirika pale Algeria ilipopoteza mechi dhidi ya Ivory Coast katika robo fainali ya Kombe la mataifa ya Afrika alipokuwa akikabwa zaidi kila alipokuwa akicheza.
Alichezewa visivyo mara saba wakati Ivory iliposhinda kwa magoli 3-1 na visa hivyo vikiongezeka sana kutoka kwa kiwango cha wastani cha mara 3.7 alizofanyiwa madhambi katika hatua ya makundi, ambako Algeria ilikuwa imeibuka imara kutoka katika kundi la kifo.
Licha ya kushindwa kuchukua kombe Brahimi ameendelea kung’ara kila siku.
WASIFU WA YAYA TOURE;
Ndoto ya mchezaji wa Ivory Coast na
Manchester Yaya Toure hatimaye ilitimia mwaka 2015, jaribio la sita,
alipolinyanyua Kombe la Taifa Bingwa Afrika.
Waliishinda Ghana kwa matuta hayo baada ya fainali kuisha sare tasa, Toure akifungwa mkwaju wake.
Yaya alikuwa kijana mdogo mwenye umri wa miaka minane tu wakati Ivory Coast waliposhinda Kombe la Taifa Bingwa Afrika mara ya kwanza 1982. Mwanasoka huyu hodari sasa aliwaongoza kushinda kombe hilo mara ya pili, akiwa nahodha wao.
Ilikuwa ni ushindi zawadi mwafaka kwa mmoja wa wachezaji bora zaidi wa kandanda kuwahi kutoka Afrika na idhinisho kwa kizazi cha wachezaji ambacho kilikuwa na uwezo mkubwa.
"Tangu mwaka wa 2006, watu walikuwa wakisema kuwa Ivory Coast ni timu bora lakini hatukufanikiwa,” Toure ambaye aliweza kushirikishwa kwa mara ya tatu kwenye timu bora ya dimba, aliiambia BBC Sport.
"Mwaka 2015 ulikuwa mwaka mzuri sana kwa sababu tulikuwa pamoja na kakangu (Kolo), na kuyanyua kombe kama nahodha, kulinifurahisha zaidi.
Akiwa na mchezo wake imara kama kawaida, Toure aliwatia moyo wenzake, akawaongoza kutoka safu ya kati na kutoa kombora kali wakati wa nusu fainali dhidi ya DR Congo.
Baada ya kurejea Abidjan kwa shangwe kama washindi, ni mshindi huyu tuzo ya BBC ya mwanakandanda bora wa Afrika wa mwaka 2013 aliyepewa jukumu la kutua na kombe kutoka uwanja wa ndege, kiongozi wa timu iliyokuwa imempoteza Didier Drogba aliyestaafu miezi michache awali.
Huku kombe hilo likiendelea kuonyesha zaidi mchango wake kwa taifa, lilisisitiza umuhimu wake kwa klabu yake.
Kabla ya kuondoka kushiriki fainali za kombe hilo, City walikuwa wameshikila nafasi ya kwanza katika ligi ya Uingereza, Toure akiwa ameshirki katika michezo tisa na kuwasaidia kushinda michezo yote tisa.
Bila yeye, miamba hawa wa Manchester hawakuweza kushinda mechi tano zilizofuata, wakateleza katika kinyang’anyiro chao cha kusaka taji la Ligi ya Premia na pia wakabanduliwa Kombe la FA.
Walimaliza msimu wa 2014/2015 bila kikombe chochote, na licha ya kukosa ligi miezi miwili akishiriki Kombe la Taifa Bingwa Afrika, raia huyo wa Ivory Coast alikuwa mmoja wa wachezaji watatu pekee waliofunga mabao 10 na zaidi (wengine wakiwa Sergio Aguero na David Silva)
Mchezaji huyu wa umri wa miaka 32 alianza msimu huu vyema hata zaidi, akiongoza City kutulia kileleni na kuanza kila mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya na mwishowe klabu hiyo ikafika hatua ya makundi.
Oktoba, alifanikiwa kuwa miongoni mwa walioteuliwa kuwania tuzo ya Fifa Ballon d’Or, inayotambua mchezaji bora wa mwaka, kwa mwaka wa nne mtawalia. Kwa miaka mitatu iliyopita, amekuwa ndiye Mwafrika pekee kwenye orodha hiyo.
Hili wa kiasi kikubwa ni kwa sababu Toure ni mchezaji mzuri sana, mara nyingi huwa anaonekana kama mtu mzima akishindana na watoto uwanjani, anavyocheza kwa urahisi dhidi ya wapinzani wake na kusonga na mpira.
City ilikuwa haijashinda kombe lolote kwa karne nne kabla ya mchezaji huyo wa zamani wa Barcelona kujiunga nao mwaka 2010. Tangu wakati huo, wameshinda mataji mawili ya Ligi ya Premia, Kombe la Ligi na wamekuwa wakicheza soka ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni