WATAKAO WANIA TUZO YA MWANASOKA BORA ZAIDI AFRIKA 2016;
Wasifu wa Sadio Mane
Mchezaji soka wa kimataifa wa taifa la Senegal Sadio Mane amekuwa na mwaka wa mafanikio.
Kasi yake, vile anavyodhibiti mpira mbali na anavyofikiria kwa haraka ni suala ambalo huzua hofu miongoni mwa wapinzani wake hatua ambayo imemfanya kuvutia nyoyo za mashabiki na kupata sifa kutoka kwa wataalamu wa soka.
Ni mchezaji mwenye ujanja mwingi sana na ambaye ni mwepesi mbele ya lango mbali na kuweza kuchukua pasi na kutengeza nafasi kwa wachezaji wenza.
Mady Toure, mwanzilishi wa Academie Generation foot, ambapo Mane alianza elimu yake ya soka, anaamini kuwa Mane ni mchezaji aliyetimia.
"Sadio Mane ana kitu ambacho hata Lionel Messi hana, kitu ambacho hata Neymar hana," aliambia BBC michezo.
Mane alimaliza msimu uliopita akiwa mfungaji bora wa Southampton akiongoza na mabao 15 katika mashindano yote na akafanikiwa kupata uhamisho kwenda Liverpool kwa kitita cha pauni milioni 34.
Uhamisho huo hadi Liverpool ulimfanya kuwa mchezaji ghali zaidi wa Afrika katika historia, huku fedha za uhamisho wake zipiku zile ambazo klabu ya Manchester City iliilipa Swansea ili kumnunua mshambuliaji Wilfried Bony mnamo mwezi Januari 2015.
Mane ana mabao sita na amsaidia ufungaji wa mabao 11 kwa Liverpool msimu huu.
Amekuwa aking'ara tangu ajiunge na Liverpool, ambapo alifunga katika mechi yake ya kwanza na Liverpool katika ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Arsenal katika mechi ya ufunguzi wa msimu.
Mane alionyesha umahiri wake tena kwa kufunga bao moja huku akitengeza jingine katika mechi iliofuata, na mechi nyengine Mane alitengeneza nafasi mbili za mabao huku Liverpool ikiicharaza Burton Albion 5-0 katika mechi ya kombe la ligi.
Alithibitisha uwezo wake katika kufunga mabao kwa kufunga bao moja na kusaidia ufungaji wa jingine katika ushindi wa nyumbani wa 4-1 dhidi ya mabingwa watetezi wa ligi, Leicester mbele ya mashabiki wao.
Mabao yake mengine yalitokana na mechi za ligi katika ushindi dhidi ya Hull City na West Brom na hivi karibuni alifunga mabao mawili katika ushindi wa 6-1 dhidi ya Watford.
Katika safu ya kimataifa, Mane alikuwa nyota wa Senegal katika mechi ya ufunguzi wa kufuzu katika kombe la dunia la mwaka 2018 mnamo mwezi Oktoba, akithibitisha kuwa mchezaji muhimu na vilevile akafanikiwa kufunga bao muhimu katika mechi dhidi ya Cape Verde.
Akiwa amechezeshwa mara 36 na taifa lake, Mane anajivunia mabao 10 na kutoa usaidizi wa mabao 11 kwa timu ya Simba wa Teranga na atakuwa kiungo muhimu katika matumaini yao ya kufuzu kwenda Urusi 2018 pamoja na Kombe la Taifa Bingwa Afrika mwakani nchini Gabon.
Mchezo wa Mane katika klabu yake na taifa umemfanya kuwa na thamani kubwa katika orodha ya mgombea wa mchezaji bora wa BBC wa mwaka, kwa mwaka wa pili mfululizo.
Tayari uamuzi wake wa kuacha shule akiwa umri wa miaka 15 na kuanza kucheza soka ya kulipwa umempatia ufanisi mkubwa.
Alishinda taji la ligi na lile la kombe la ligi mara mbili akiichezea timu ya FC Salzburg ya Austria 2014 .
Ni mshambuliaji wa Senegal anayetegemewa sana na mnamo mwezi Mei 2015 aliweka rekodi mpya ya kufunga mabao matatu kwa haraka katika historia ya ligi hiyo wakati alipofunga hatrick (mabao matatu mechi moja) katika sekunde 175 akiichezea Southampton dhidi ya Aston Villa.
Akianza soka yake huko Sidhiou hadi katika ligi ya Uingereza kupitia Dakar, Ufaransa na Austria safari ya Mane imejaa bashasha.
Na ukweli ni kwamba ana uwezo wa kuwa mchezaji bora wa Afrika atakayeenziwa.
Piga kura hapa : bbc.com/africanfootball
Wasifu wa Pierre-Emerick Aubameyang
Tangu alipoanza kucheza, mshambuliaji huyu wa Borussia Dortmund, mzaliwa wa Gabon alishamiri.
Alisajiliwa kama mchezaji wa AC Milan ya Italia ambayo hata hivyo hakuichezea kwani alipelekwa kwa mkopo katika timu ya Dijon ya Ufaransa.
Na katika mechi yake ya kwanza ya kirafiki kabla ya msimu kuanza, kijana huyo aliyekuwa na umri wa miaka 18 aliwashtua wakubwa zake.\
"Unapocheza mechi hiyo ya kwanza ya msimu unakua bado hauko tayari, lakini hata hivyo yeye tayari alikuwa bora na mwepesi kuliko wengine," anasema Flirent Perraud, ambaye wakati huo alikuwa mlinda lango wa timu ya Dijon.
"Uwanjani, tulikuwa tukisema, 'kijana huyu ni nani? ni mchezaji wa ajabu tuliyepewa'.
"Tuligundua kwamba kumbe siyo mtoto mdogo bali mchezaji wa ajabu."
Katika msimu wake wa kwanza kama mchezaji wa kulipwa Aubameyang alifunga magoli 10.
Halafu kijana huyo aliyekulia Ufaransa akaanza ziara ya kufana iliyompeleka Colombia, Italia na Mexico (akimfuata mwanasoka Babake Pierre) na wakati huo alihamishwa kwa mkopo katika timu za Lille, Monaco na St Etienne iliyompa mkataba wa kudumu mwaka 2011 na ambapo mchezo wake ulianza kuimarika.
Kutoka huko, kuhamia kwake katika timu ya Dortmund mwaka 2013 kuliharakisha mwendo wake wa kuwa mmoja kati ya washambuliaji wazuri duniani.
Mwezi Juni mwaka 2016 alikuwa Mwafrika wa kwanza kupewa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa ligi kuu ya soka ya Ujerumani - Bundesliga - kufuatia kura inayopigwa na wachezaji wenzake.
Fomu yake pia ilimwezesha 'Auba' kama mchezaji wa kwanza raia wa Gabon kushinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka barani Afrika ya CAF, na kuwekwa kwenye orodha ndogo ya FIFA ya kuwania kuwa mchezaji bora wa mwaka 2016.
Kimsingi anafahamika kwa upachikaji wake wa magoli.
Ameshanusa nyavu mara 11 katika mechi 9 za Bundesliga, yakiwemo magoli 4 aliyofunga waliposhinda Hamburg 5-2 .
Kwa ujumla ameshaifungia Dortmund magoli 89 katika mechi 152.
Kuna pia kasi yake ambayo ni kubwa ukilinganisha na Usain Bolt katika masafa mafupi, bila kusahau namna yake ya kusherehekea baada ya kufunga goli, mfano wa Batman na Spiderman.
"Anapenda utani na kuchekesha watu, ni kijana mcheshi, rafiki mzuri kabisa," anasema Jordan Loties waliyecheza pamoja katika timu ya Dijon.
Mitindo ya mavazi na nywele zake inaonyesha kwamba kweli Aubameyang ni mtu wa kuvutia ijapokuwa mwenyewe anajieleza kama mwenye kuona haya.
"Nilifanya kazi kwa bidii kufikia kiwango hiki," Aubameyang aliambia BBC.
Mwanasoka kijana, aliyebuni viwanja mfano katika chumba chake kabla ya kuwakilisha timu ya vijana ya Ufaransa, Aubameyang alifuata nyayo za Babake kuwa nahodha wa timu ya taifa ya Gabon maarufu 'Chui'
"Nilichagua Gabon ili kuiwakilisha Afrika na kuchukua nafasi ya Didier Drogba na Samuel Eto'o," alisema.
"Lakini kufanya hivyo, huna budi kushinda tuzo."
Tayari ana msururu wa tuzo, je tuzo ya BBC itaongezeka katika kabati lake la vikombe?
Piga kura hapa : bbc.com/africanfootball
Wasifu wa Riyad Mahrez
"Utadhani ameweka gundi katika mguu
wake kutokana na vile mpira unavyokwama''. Hayo yalikuwa maoni ya awali
ya rafikiye mgombea wa taji la mchezaji bora wa mwaka 2016 barani Afrika
Riyad Mahrez, Madjid.
''Sasa dunia nzima inafahamu uwezo wa Mahrez wa kuucheza mpira anavyotaka na sasa ni klabu kubwa duniani wala sio vijana wenzake wanaotaka ajiunge nao''.
Baada ya kuisaidia Leicester kushinda taji la ligi kuu nchini Uingereza mwaka 2016, katika kile kilichoonekana kuwa kisa cha kushangaza na cha kihistoria, klabu za Arsenal, Barcelona na Chelsea zilitaka kumsajili.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Algeria alikuwa ametangazwa kuwa mchezaji wa kulipwa wa mwaka, akiwa raia wa kwanza wa Afrika kupata taji hilo baada ya kuanzisha kampeni hiyo akicheza wingi ya kulia kwa kufunga mabao 17 kutoa usaidizi wa mabao mara 11 katika mechi 34 za ligi kuu.
Ulikuwa msimu ambapo Mahrez ambaye alijiunga na Leicester kutoka Le Havre kwa pauni 400,000 pekee mwaka 2014, aliimarika na kuisaidia timu yake pamoja na yeye mweyewe kufaidika zaidi ya ndoto yao.
Pengine siku iliyong'arisha nyota ya mchezaji huyo inayopaswa kuwekwa katika kumbukumbu ilikuwa Februari 6 nyumbani kwa mabingwa watetezi wa ligi ya Uingereza Manchester City wakati Mahrez alipougusa mpira na kumpita Nicolas Otamendi, akamchenga Martin Demichelis kabla ya kupiga mkwaju mkali katika lango la Man City ulioiweka Leicester kifua mbele 2-0.
Leicester ilishinda mechi hiyo 3-1 huku Mahrez akisaidia kupata mabao matatu katika mechi nyingine hatua ambayo iliisadia timu hiyo kuwa na ufanisi mkubwa na kushinda ligi.
Ni kwa sababu hiyo ndio maana hakuwashangaza wengi alipoanza kusakwa na klabu kubwa.
Timu zilianza kuitafuta saini ya mchezaji huyo mwembamba kwa maumbile, mchezaji ambaye umahiri wake umeleta hewa safi katika wingi na kuwafurahisha mashabiki na amekuwa tegemeo la wenzake.
Lakini mchezaji huyo amekataa kujiunga na klabu hizo kubwa na kusema kuwa alitaka kucheza katika klabu hiyo kwa msimu mwengine ili kuthibitisha uwezo wake.
Ameifungia Leicester mabao manne tayari msimu huu matatu kati yao yakitoka katika ligi ya vilabu bingwa ulaya.
Na amekuwa kiungo muhimu katika kuhakikisha kuwa Algeria inafuzu katika michuano ya kombe la mataifa bingwa Afrika itakayochezwa nchini Gabon.
''Riyad anaifanya timu yake ya taifa kuwa kubwa. Kila mtu anaijua Algeria kutokana na umaarufu wa Riyad." alisema mchezaji mwenza wa Algeria Mehdi Abied.
''Nchini Algeria tunajivunia sana Riyad. Sio rahisi kuwa mchezaji bora wa ligi ya Uingereza. Ni kitu kikubwa sana''.
"Kila mtu barani Afrika anampenda Riyad. Nakumbuka tulienda Ethiopia na Algeria na walikuwa wanamshabikia Riyad zaidi ya wachezaji wa timu yao''!
Piga kura hapa : bbc.com/africanfootball
Wasifu wa Andre Ayew
Mchezaji wa kimataifa wa Ghana Andre Ayew ameonyesha kwamba siyo mtu wa kuogopa matatizo.
Mtazamo wake chanya na mwendelezo wa kucheza vizuri na kufunga magoli siyo tu ulimsaidia yeye binafsi bali pia uliisaidia timu yake katika kupambana isishuke kutoka ligi kuu ya Uingereza.
Ayew alifunga magoli 2 walipoishinda Liverpool 3-1 na kusaidia timu ya Swansea kupata matokeo mazuri ambayo hatimaye yalithibitisha kusalimika kwake baada ya kampeni iliyokuwa ngumu.
Kwa hivyo siyo jambo la kushangaza kuona kwamba alishinda tuzo ya klabu hiyo ya mchezaji mgeni wa mwaka baada ya msimu.
Fomu yake ilikuwa ya kuvutia kiasi kwamba, mwezi Agosti timu ya West Ham ya mashariki ya jiji la London ilivunja rekodi yake kwa kumsajili Ayew kwa kitita cha pauni milioni 20.5.
Ayew hakuwa na bahati kwani alijeruhiwa vibaya katika mechi yake ya kwanza akiichezea Hammers lakini kadiri atakavyoshiriki mechi nyingi hakuna shaka atathibitisha ada ya uhamisho wake.
Baada ya miezi miwili ya kukosekana kwake alirejea uwanjani mwishoni mwa mwezi Oktoba.
Na "machoni anaonekana mwenye uchu" kama alivyoona mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Ghana Yaw Preko mara ya kwanza walipocheza pamoja na kuwa ndicho kitakachomsaidia kudhihirisha thamani yake kwa timu yake mpya msimu ujao.
Wakati huo huo, kimataifa Ayew ameendelea kuwa mchezaji muhimu kwa timu ya taifa ya Ghana mwaka 2016.
Alikuwa miongoni mwa wafungaji Ghana ilipoilaza Mauritius 2-0 na kutangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo ambapo Black Stars walijikatia tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Taifa Bingwa Afrika mwakani nchini Gabon.
Na kulipokuwa na kipindi kigumu mwaka 2016 cha majeraha na matatizo mengine ya timu, Ayew alijituma kama kawaida yake.
Lakini katika maisha yake Ayew ni mtu aliyezoea kukabiliana na presha na matarajio ya wengi kwa kuwa mtoto wa gwiji wa zamani wa Ghana, Abedi Pele Ayew ambaye anachukuliwa kuwa mmojawapo wa wachezaji bora wa Afrika wakati wote.
Babake Ayew aliichezea Black Stars mara 73 na kufunga magoli 33 huku akiisaidia kutwaa ubingwa wa Afrika mwaka 1982 na kunyakua nafasi ya pili mwaka 1992.Pia mwaka 1993 alishinda kombe la klabu bingwa Ulaya akichezea Marseille.
Miaka miwili kabla alikuwa amepoteza fainali ya kombe la Ulaya.
Mengi ya kusisimua sasa
Lakini Ahmed Brynes, mkufunzi wa Nania FC ya Ghana ambako Ayew alianzia kufuata nyayo za babake alitoa ubashiri wake wa kuvutia."Ayew alipokuwa tu na umri wa miaka 14, alikuwa mchezaji wa ajabu na tena alikuwa akisema 'nataka kuwa bora zaidi kuliko babangu," Brynes aliambia BBC.
"Nilimwambia,'angalia babako alifika kiwango cha juu sana kuliko wewe'....lakini akajibu 'nitampita' na nina uhakika atapita kiwango hicho."
Abedi Pele Ayew alishinda tuzo ya mchezaji bora wa Afrika mwaka 1992.
Kijana wake Ayew akaiga mfano wake mwaka 2011-Je, mwaka huu ndio unaweza kuwa wa kumpita?
Piga kura hapa : bbc.com/africanfootball
Wasifu wa Yaya Toure
Yaya amewahi kushinda Tuzo ya BBC ya
Mwanakandanda Bora wa Afrika wa Mwaka mara mbili na ni mshindi mara nne
wa taji la mchezaji bora wa mwaka wa taji linalotolewa na shirikisho la
soka barani Afrika (CAF), kwa hivyo haishangazi kumuona tena katika
orodha ya wanaogombea taji hilo.
Na hata kama anaendelea kucheza, mchango wake unatambulika.
Mnamo mwezi Februari aliishindia klabu yake ya Manchester City kombe la Ligi alipofunga penalti ya pekee kuishinda Liverpool katika fainali.
Pia ameisaidia klabu yake kufika robo fainali Kombe la Klabu Bingwa Ulaya na kumaliza katika nafasi ya nne katika ligi ya Uingereza ili kuhakikisha kuwa timu hiyo inawakilishwa tena Kombe la Klabu Bingwa Ulaya .
Ufanisi huo ulimaanisha kwamba Toure aliamua kusalia na kupigania nafasi yake katika kikosi cha City licha ya kuwasili kwa Pep Guardiola ambaye alichangia kuondoka kwake katika timu ya Barcelona wakati alipokuwa mkufunzi wa timu hiyo.
Lakini wakati matamshi ya ajenti wake Dimitri Seluk kwamba mchezaji huyo ananyanyaswa wakati alipoachwa nje katika kikosi cha michuano ya Kombe la Klabu Bingwa Ulaya msimu huu, mchezaji huyo aliachwa nje kabisa ya kikosi cha Manchester City na hajakuwa akichezeshwa.
Mkufunzi huyo alisema kuwa Toure hatoshiriki mechi za klabu hiyo hadi pale ajenti wake atakapoomba msamaha, ijapokuwa hilo halijatekelezwa, Toure mwenyewe ameomba msamaha.
Ijapokuwa Toure hapendezwi na hatua ya kuwekwa nje ya kikosi cha City, uamuzi wake wa kurudi katika soka ya kimataifa mwaka 2016 ni wake mwenyewe.
Alichukua takriban miezi 18 kufanya uamuzi huo kufuatia ushindi wa taifa lake katika michuano ya mataifa ya bara Afrika huko Equatorial Guinea.
Kocha wa zamani wa timu ya taifa lake Francois Zahoui alikuwa mongoni mwa wale walio jaribu kumshawishi kuendelea na harakati za kuisaidia timu yake ya taifa kufuzu kwa kombe la mataifa ya bara Afrika 2017 nchini Gabon pamoja na kombe la dunia la mwaka 2018 nchini Urusi.
Sio vigumu kujua kwa nini.
Huku akiwa amechezea timu yake ya taifa mara nyingi zaidi ,Toure amekuwa kiungo muhimu katika timu ya Ivory Coast na aliimarisha ufanisi wake katika timu ya taifa kwa kuisaidia kushinda taji la Afrika la mwaka 2015.
Pia ameshiriki katika kila mechi ambayo Ivory Coast imecheza ikiwemo kushiriki mara tatu kwa timu hiyo katika michuano ya Kombe la Dunia.
Ni mwaka 2016 alipogundua kwamba ni wakati wa kustaafu katika soka ya kimataifa ijapokuwa hajatoa uamuzi wake wa mwisho.
„Ujumbe huo ulikuwa mgumu katika maisha yake," ,alisema katika taarifa yake ya kustaafu Septemba iliopita.
Lakini aliweka wazi kwamba hafikirii kwamba mchezo wake unaendelea kudorora.
''Suala kwamba mimi nina umri wa miaka 33, ugumu wa mazoezi na wingi wa mechi sio sababu kwamba ninachukua uamuzi huu," alisema.
Piga kura hapa : bbc.com/africanfootball
Kanuni na Masharti ya Tuzo ya BBC ya Mwanakandanda Bora wa Afrika wa Mwaka 2016
Orodha ya wachezaji watakaopigania Tuzo ya BBC ya Mwanakandanda Bora wa Afrika wa Mwaka 2016 itatangazwa kwenye kipindi maalum cha moja kwa moja cha Mchezaji wa Afrika wa Mwaka katika BBC World Service, BBC World News, mitandao ya BBC na katika mitandao ya kijamii. Kipindi hiki kitapeperushwa saa 1805GMT hadi 1900 GMT mnamo Jumamosi Novemba 12. Ukurasa wa kupigia kura utafunguliwa takriban saa 1850GMT.
Maelezo na utaratibu wa kupiga kura ni kama ifuatavyo.
Shughuli ya kuchagua wachezaji wa kushindania
Orodha ya wachezaji watano wa kushindania tuzo hii ilitayarishwa na wataalamu bingwa wa soka Afrika, ambapo mtaalamu mmoja kutoka kila nchi aliombwa kutaja wachezaji watatu anaohisi wanafaa kushindania, bila kufuata utaratibu wowote katika kuwataja wachezaji hao watatu.Waliombwa kuteua wachezaji wao kwa kufuata mambo yafuatayo: ustadi wa kibinafsi; uwezo wa kiufundi; kufanya kazi na timu; mchango katika matokeo na kucheza kwa njia ya haki, zilizoonyeshwa wakati wa msimu wa 2015/16.
Majina ya wachezaji watakaoshindania tuzo yatatangazwa wakati wa kipindi cha moja kwa moja runingani na redioni mnamo Jumamosi 12 Novemba kuanzia saa 1805-1900 GMT katika BBC World Service na BBC World TV. Majina yatatangazwa pia katika www.bbc.com/africanfootball.
Ikitokea kwamba kuwe na wachezaji waliotoshana kwa kura wakati wa uteuzi, kundi la waandalizi wa Tuzo ya Mwanakandanda Bora wa Mwaka wa Afrika ina haki ya kuongeza orodha ya wachezaji wa kushindania tuzo hadi wachezaji sita.
Nani anastahili kushindania
Watu wamehitimu kushindania Tuzo ya Mwanakandanda Bora wa Afrika wa Mwaka iwapo wanahitimu kuchezea timu ya taifa lolote la Afrika.Umma kupiga kura
Majina ya wachezaji watakaoshindania tuzo yatakapochapishwa, mshindi wa tuzo ataamuliwa kupitia kura za umma mtandaoni.Shughuli ya upigaji kura itafunguliwa takriban saa 1850 GMT mnamo Jumamosi 12 Novemba 2016 na kufungwa saa 1800 GMT mnamo Jumatatu 28 Novemba 2016.
Matokeo ya mwisho yatatangazwa saa 17:35 GMT mnamo Jumatatu Desemba 12, moja kwa moja katika runinga ya Focus on Africa na redio. Mshindi pia atatangazwa kwenye ukurasa wa Mchezaji Bora wa Afrika wa BBC pamoja na kanuni na masharti yanayotumika.
Ikitokea kwamba wachezaji watoshane kwa kura, wachezaji hao watatunukiwa tuzo kwa moja.
Jinsi ya kupiga kura - mtandaoni
Kwa kutembelea ukurasa wa Mwanakandanda Bora wa Afrika wa Mwaka katika www.bbc.com/africanfootball na kufuata maagizo mtandaoni. Kompyuta moja inaweza tu kutumiwa kupiga kura mara moja.
Kura ya umma - Kanuni na masharti
1. Kura hii inaendeshwa na BBC na tuzo hii imetimiza viwango na matakwa ya mwongozo wa maadili wa BBC kuhusu kufanywa kwa mashindano & kura ambao unaweza kupatikana www.bbc.co.uk/editorialguidelines/guidelines/appendix22. Mshindi atapokezwa kikombe kilichoandikwa jina na atunukiwe taji la Mwanakandanda Bora wa Afrika wa Mwaka wa BBC 2016.
3. Orodha ya wachezaji watakaoshindania Tuzo ya BBC ya Mwanakandanda Bora wa Afrika wa Mwaka itaandaliwa na wataalamu wa soka kutoka Afrika.
4. Utaratibu uliofuatwa kupata majina haya ni kama ifuatavyo: ustadi wa kibinafsi; uwezo wa kiufundi; kufanya kazi na timu; mchango katika matokeo na kucheza kwa njia ya haki, zilizoonyeshwa mwaka 2016.
5. Majina ya wanaoshindania tuzo yatawekwa wazi kwa umma wapigiwe kura kupitia tovuti ya Mwanakandanda Bora wa Afrika wa Mwaka katika www.bbcworldservice.com/africanfootballer na www.bbc.com/africanfootball. Kompyuta moja itaruhusiwa kupiga kura moja pekee mtandaoni..
6. BBC itatumia maelezo ya mtu binafsi kwa minajili ya kufanikisha upigaji kura pekee na haitayachapisha au kuyawasilisha kwa mtu mwingine yeyote yule bila idhini yako. Iwapo ungependa kufahamu zaidi kuhsuu sera ya faragha ya BBC, tafadhali tazama Sera ya Faragha ya BBC katika www.bbc.co.uk/usingthebbc/privacy.
7. Muda wa mwisho kupiga kura ni saa 1800 GMT mnamo Jumatatu 28 Novemba 2016.
8. Uamuzi kuhusu kura zitakazopigwa ni wa mwisho na hakutakuwa na mawasiliano ya ziada..
9. Tuzo lazima ipokelewe kama ilivyoelezwa na haiwezi kuahirishwa. Hakutakuwa na malipo yoyote ya kifedha mbadala. Hakutakuwa na malipo kwa sababu ya kupiga kura.
10. BBC, watu waliopewa kandarasi na BBC, kampuni tanzu na/au mawakala hawawezi kukubali lawama kwa matatizo yoyote ya kiufundi au matatizo mengine yoyote kuhusiana na kufikia huduma ya mtandao, mfumo wa mtandao, sava, mtoaji huduma ya mtandao au mambo mengine ambayo huenda yakasababisha kura kupotea au kutonakiliwa au kusajiliwa vyema.
12. BBC inabaki na haki ya kubatilisha kura zilizowasilishwa au kusitisha upigaji kura kukitokea sababu za kutosha za kushuku kwamba ulaghai umetokea katika upigaji kura au ikishuku kwamba kumekuwa na jaribio la wizi wa kura. BBC ina haki ya kutoa njia mbadala ya kufanya uteuzi bila kuomba ushauri kutoka kwingineko.
BBC haitachapisha habari na maelezo au kuwasilisha maelezo hayo kwa mtu yeyote bila idhini, ila tu katika hali ambapo yanahitajika katika kutekeleza masharti haya. Kwa maelezo zaidi, tafadhali tazama: Sera ya Faragha ya BBC http://www.bbc.co.uk/usingthebbc/privacy/
13. Wale wanaoshiriki katika kura hii, wote wanachukuliwa kwamba wamekubali kanuni hii na wanafungamanishwa nazo. Tafadhali, fahamu kwamba mfanyakazi wa BBC au mtu mwingine yeyote ambayo naahusika kwa njia moja ama nyingine katika maandalizi ya utoaji wa Tuzo hii haruhusiwi kupiga kura.
14. Upigaji kura wote utasimamiwa na BBC Africa.
16. BBC inabaki na haki ya kumuondoa mchezaji yeyote anayeshindani au kutokabidhi tuzo iwapo itabaini, kwa uamuzi wake mwenyewe, kwamba mchezaji huyo kuendelea kushiriki au tuzo hiyo kutolewa, kunatishia kuishushia hadi BBC.
17. Kanuni hizi zimo chini ya sheria za England na Wales.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni