MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka mashabiki
wa soka nchini kutambua kuwa inalijadili kwa kina tukio la kukamatwa kwa basi
lililokuwa limebeba wachezaji wa timu ya Serengeti juzi.
Juzi basi lililokuwa limebeba wachezaji wa timu hiyo
majira ya jioni katika eneo la Kisutu lilikamatwa na kampuni ya Udalali ya TRA,
Yono Auction Mart wakati likiwapeleka wachezaji hao kwa Makamu wa Rais kwa
ajili ya chakula cha usiku.
Msemaji wa TRA, Richard Kayombo alisema kuwa Mamlaka
hiyo imesikitishwa na kitendo hicho na kuwa inaendelea na mazungumzo ya ndani
kuona ni hatua gani ya kuchukua.
Alisema, TRA ni sehemu ya wananchi na timu hiyo ni
timu ya wananchi ambapo imekuwa ikijiandaa kuiwakilisha nchi kwenye fainali za
Kombe la Mataifa Afrika kwa wachezaji wenye umri wa chini ya miaka 17.
Aliongeza kwa namna yoyote ile wachezaji hao
hawakutakiwa kubugudhiwa kiakili na kwa kitendo cha kushushwa kwenye basi kwa
kuwa ni Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) ndio linalodaiwa.
“Tunapenda kuwaomba radhi na pia kulaani kwa kitendo
kile kwa kuwa kwanza sio uungwana na pili ilitakiwa kutumika kwa hekima zaidi
na sio kile kilichofanyika pale, kwa kweli TRA inalifuatilia kiundani suala
hilo kwa sasa” alisema Kayombo.
Akizungumza na gazeti hili Mkurugenzi wa Yono
Auction Mart, Stanley Yono alisema kuwa kampuni yake ilikuwa ikitekeleza
maagizo ya serikali ya kukusanya wadaiwa wa TRA.
“Kwa sasa ninachoweza kusema ni kuwa maafisa wa kampuni
hii walikuwa kwenye utekelezaji wa majukumu yao na hiyo ilikuwa ni sehemu ya
kazi hiyo” alisema Yono.
Timu hiyo imeondoka jana mchana kuelekea nchini
Morocco kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya kujiandaa na Kombe la Mataifa ya
Afrika kwa Vijana itakayofanyika nchini Gabon mwezi Ujao.
TRA
imezifungia ofisi za TFF kwa kile kinachodaiwa
kuwa ni malimbikizo ya kodi za mishahara ya aliekuwa kocha wa Timu ya
Taifa, Marcio Maximo kwa miaka minne tangia mwaka 2006 hadi 2010.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni