RAIS wa Simba SC, Evans Aveva amemuandikia barua
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Simon Sirro kuomba kufanya
maandamano ya amani kupinga kile wanachoamini uonevu wanaofanyiwa na Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF).
Katika barua hiyo, ambayo nakala yake imetumwa pia kwa Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo, Aveva amesema kwamba wanataka waandamane Jumanne ya Aprili 25, mwaka huu.
Aveva amesema wanataka maandamano hayo yatakayohusisha wanachama wote wa Simba, yaanzie makao makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Msimbazi hadi Wizara ya Habari.
“Lengo la maandamano hayo ni kupeleka ujumbe kwa
shirikisho hilo, ambalo limekuwa likifanya uonevu katika maamuzi yake dhidi ya
klabu ya Simba. Ifahamike kuwa malalamiko mengi ya klabu ya Simba yamekuwa
hayasikilizwi kwa kipindi kirefu,”amesema Aveva.
Lakini pia Aveva amesema wana taarifa Msemaji wao, Hajji Manara ameitwa kwenye Kamati ya Maadili kwa kile kinachoonekana kutaka kumfungia na kumziba mdomo ili asiweze kuongeela uonevu huu.
“Ni matumaini yetu kuwa jeshi lako litatoa ulinzi wa kutosha kwa wanachama na mashabiki wetu,”amesema Aveva katika barua yake hiyo kwenda kwa Kamanda Sirro.
Maombi hayo yanakuja muda mfupi baada ya TFF kumtaka Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Hajji Sunday Manara kufika Kamati ya Maadili Aprili 21, 2017 kujibu tuhuma za utovu wa nidhamu dhidi ya viongozi wa Shirikisho hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni