Timu ya soka ya Simba ya jijini Dar es Salaam imeongeza wigo wa alama nane dhidi ya mpinzani wake Dar Young Africans baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mbeya City, katika mchezo wa ligi raundi ya 24 uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa.
Katika mchezo huo ambao ulikuwa mkali na wakusisimua, umeshuhudia Mganda Emmanuel Okwi akifunga bao lake la 18 msimu huu na kuendelea kukikaribia kiatu cha mfungaji bora.
Okwi amefunga bao lake katika dakika ya 14 na kumfanya kufikisha mabao 21 katika mashindano yote msimu huu, mabao ambayo pia yamemfanya kuwa mfungaji mwenye mabao mengi mpaka sasa katika mashindano yote yanayoratibiwa na TFF.
Mabao mengine ya Simba yamefungwa na Asante Kwasi katika dakika ya 32 pamoja John Raphael Bocco katika dakika ya 36 na kumfanya kufikisha mabao 13 ya ligi, huku bao pekee la Mbeya City 'Wanakomakumwanya' likifungwa na Frank Ikobela katika dakika ya 34.
Sasa Simba wanafikisha alama 55 na kuwaacha Solemba watani zao Yanga waliokatika nafasi ya pili na alama zao 47 Licha ya mnyama kuwa mbele kwa mchezo mmoja.
Mtibwa 1-0 Ndanda
Matokeo mengine, Mtibwa Sugar wameibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Wanakuchele Ndanda FC katika mchezo ambao umefanyika katika uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro.
Bao pekee la Mtibwa Sugar limefungwa na Kelvin Sabato katika dakika ya 22 ya mchezo huo ambao ulikuwa mkali licha ya kuharibiwa na hali ya uwanja kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Ruvu Shooting vs Azam
Mchezo kati ya Ruvu Shooting na Azam uliopangwa kufanyika Leo saa nane mchana, umeahirishwa kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha katika maeneo ya Mlandizi na kufanya uwanja kushindwa kuchezewa, sasa mchezo huo utapigwa kesho saa nne asubuhi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni