Hata hivyo, uchaguzi wa klabu hiyo ambao ulikuwa umepangwa kufanyika
mwezi huu, umesogezwa mbele kwa mwaka mmoja kutokana na uamuzi wa
Mkutano Mkuu uliofanya maboresho ya Katiba, Uamuzi huo ulilenga
kumwongezea Manji na uongozi wake muda wa mwaka mmoja hadi Juni mwakani.
MWENYEKITI wa Yanga, Yusuf Manji, ametimiza miaka miwili sasa tangu
alipoingia madarakani mwaka 2012 katika uchaguzi mdogo wa klabu hiyo na
Juni hii ndiyo ilikuwa mwisho wa awamu ya uongozi wake.
Hata hivyo, uchaguzi wa klabu hiyo ambao ulikuwa umepangwa kufanyika
mwezi huu, umesogezwa mbele kwa mwaka mmoja kutokana na uamuzi wa
Mkutano Mkuu uliofanya maboresho ya Katiba, Uamuzi huo ulilenga
kumwongezea Manji na uongozi wake muda wa mwaka mmoja hadi Juni mwakani.
Kuhusiana na hilo, Manji anasema: “Lilikuwa ni jambo la kushitukiza
kwangu, sikutegemea kama wangeamua kuniongezea muda kwani nilishaweka
azma yangu wazi kuwa nisingependa kugombea tena kwa kipindi kingine, ile
siku nilijiandaa kukabidhi ofisi na kila kitu nilishakiandaa tayari.
“Nilishtushwa zaidi walipotaka kuniongezea miaka minane, ni mingi sana,
kikubwa mimi napenda kuwaondoa shaka wana Yanga kuwa mimi naipenda klabu
hiyo, niwe Mwenyekiti au mwanachama wa kawaida, nikipenda kitu huwa
sipendi nusu, hivyo wasipate wasiwasi.”Ujio wa Maximo Manji anasema
Yanga ni timu kubwa na kocha Marcio Maximo ni mtu maarufu, wamepanga
kumtumia kuongeza wanachama wa klabu hiyo katika kampeni ya kuwataka
kuchukua kadi za uanachama zinazotolewa na Benki ya Posta Tanzania
katika mpango maalumu wa kuiongozea klabu hiyo mapato.
“Maximo atakuja kwani lengo letu ni kuhamasisha wapenzi wa klabu yetu
wajiunge na uanachama, tutamlipa ghali lakini tutahakikisha tunamtumia
kuongeza pato la klabu, si yeye pekee bali tutaleta kila mtu tunayeona
atasaidia katika hili,” anasema.
“Katika kampeni hii tutatumia pia wachezaji wetu, tutawatumia
kuhamasisha vijana wenzao kuchukua kadi za uanachama ambazo pia
mwanachama atafunguliwa akaunti kwenye benki ambayo itawasaidia kwenye
kuweka akiba.”
Vyanzo vya mapato Yanga
Manji anasema kwa sasa klabu ya Yanga inajiendesha kwa fedha za
wadhamini, viingilio vya milangoni pamoja na fedha za wafadhili na
kubainisha kuwa pato halisi la klabu hiyo linakidhi nusu tu ya mahitaji
ya klabu.
“Katika mapato kwanza, niliamua kufanya mambo kwa uwazi, matumizi ya
timu yanakaguliwa na kuchapishwa kwenye magazeti, nimeanzisha na
watakaokuja waendelee, ni changamoto,” anasema.
“Unajua ni kazi ngumu kusimamia mapato na kuyaweka kwa uwazi, lakini uzuri wake ni kwamba jambo hili linapunguza wizi wa fedha.
“Yanga inatumia Sh2.4 bilioni kwa matumizi yake ya mwaka, mapato halisi
yanayopatikana ni kiasi cha Sh1.2 bilioni tu ambacho ni nusu tu.
“Yanga ni klabu tajiri sana kutokana na kuwa na wapenzi wengi, tumeamua
kuzindua huduma ya kadi kwa wanachama ambayo ina makundi mawili tofauti,
la kwanza ni la wanachama wanaopenda kuichangia Yanga fedha nyingi na
ya pili ni ile ya kawaida ya ada ya Sh12,000 kwa mwaka.
“Kwa hiyo ya pili kila mwanachama atakatwa Sh250 kwa wiki, ni kiasi
kidogo sana ila kinamaana kubwa kwa Yanga, lengo langu ni kufanya
kampeni ili kuhakikisha tunakua na wanachama wasiopungua milioni moja
ambao wanaichangia klabu.”
Manji anabainisha kuwa baada ya mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan,
atafanya kampeni nchi nzima ili kuwahamasisha wapenzi wa klabu hiyo
kujiunga na huduma hiyo mpya.
“Nikifanikiwa kupata wanachama milioni moja hii inamaanisha kwa ada zao
pekee kwa mwezi Yanga itaingiza Sh1 bilioni kiasi ambacho ni kikubwa.
Kwa mwaka tutakua na Sh12 bilioni ambazo tukiondoa za uendeshaji wa timu
tutasaliwa na Sh9 bilioni zitakazotusaidia kujenga uwanja,” anasema
Manji
Uwanja wa Kaunda
“Tumeamua kuweka msimamo wa kutengeneza uwanja katika eneo letu la
Jangwani kutokana na ukweli kuwa ni karibu zaidi na makazi ya watu, ni
eneo ambalo watu watakwenda kutazama mpira kwa kutembea kwa miguu.
“Tunataka kujenga uwanja wenye uwezo wa kubeba watu 40,000, idadi ambayo
ni kubwa, tukienda kujenga huu uwanja nje ya mji itakua ni tatizo
kupata idadi hiyo ya watu kuja kutazama mechi zetu,” anasema Manji
Jina la uwanja kuuzwa
“Mbali na jina hata viti vya uwanjani ningependa viwe chanzo kikubwa cha
mapato, hii itakuwa kwa wanaopenda kuweka kumbukumbu zao Yanga,
tutawauzia viti kwa kuviandika majina yao, lakini akiingia uwanjani ni
lazima alipe kiingilio, jina ni kwa ajili ya kumbukumbu tu,” anasema
Manji.
Udhamini Azam TV
“Mimi na (Said Salim) Bakhresa ni marafiki, ni mfanyabiashara mwenzangu
na sina matatizo naye, wito wangu kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)
ni kuwa thamani ya Yanga ni kubwa, ni klabu yenye wapenzi wengi nchini
hivyo inapaswa kupewa fungu kubwa, mbali ya Simba, hauwezi kuifananisha
na timu nyingine yoyote.
“Tangu mechi zianze kuonyeshwa ‘Live’ katika Azam TV, ni dhahiri kuwa
mapato yameshuka, watu wengi wanaona hakuna haja ya kwenda uwanjani
wakati wanaweza kushughudia mechi kwenye luninga, hili si kwa Yanga
pekee bali ni kwa timu nyingi na rekodi zinaonyesha,” anasema Manji na
kuongeza
“Tungefanya kama Ulaya, mechi za mji huo hazitakiwi kuonyeshwa kwenye
luninga za mji, wapate kuona watu wa mikoa mingine ili wale wa mkoa
husika wajitokeze kwenda kutazama mechi uwanjani, hili litasaidia.”
“Changamoto kubwa ninayokumbana nayo ni kupata watendaji wazuri, wapo
watu wengi wanaipenda Yanga ila tatizo wanaogopa kuingia kwenye uongozi,
wanaogopa majina yao kuchafuliwa.
“Hili linachangiwa na mpira wetu kuharibiwa katika siku za nyuma,
kulikua na viongozi waliokua wakijitazama wao, waliangalia klabu
zinawafanyia nini na sio wao wanazifanyia nini klabu hizo, hilo
lilichangia migogoro na kuiporomosha heshima ya uongozi wa klabu hizi,”
anasema Manji na kuongeza
“Tatizo jingine ni matarajio makubwa wanayokuwa nayo watu juu yako,
wengi wanakutazama na usipokua makini unaweza kulewa madaraka na
kujisahau, unakua ukijiuliza jina langu litabaki vipi baada ya uongozi
wangu.
“Kila ukipita sehemu watu wanakufahamu kwa jina la Mwenyekiti, nashindwa
kutoka kwenda kupata chakula na familia yangu, mke wangu anaogopa
kutembea na mimi maana kidogo utashangaa tumepigwa picha, mama yangu
ananikana kabisa kwa kuogopa umaarufu huo, hii ni changamoto kubwa pia.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni