Beki kisiki
George Michael wa Ruvu Shooting Stars amefungiwa mechi tatu za Ligi Kuu
ya Tanzania Bara msimu huu baada ya kupatikana na kosa la kinidhamu la
kumkaba koo mshambuliaji Amisi Tambwe wa Yanga.
Baada ya kutoka suluhu dhidi ya Ruvu Shooting katika mechi yao ya raundi
ya 11 ya ligi kuu ya Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini hapa Januari
17, Yanga SC ilimfungulia mashtaka kwenye Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) beki huyo ukidai alimbagua, kumdhalilisha na kumkaba koo Tambwe.
Kamati ya Nidhamu ya TFF iliketi mwanzoni mwa wiki iliyopita na kutoa
adhabu ya kuwafungia mechi nane na tatu mabeki Juma Nyosso wa Mbeya City
FC na Aggrey Morris wa Azam FC kutokana na makosa mbalimbali ya
kinidhamu huku ikimuweka kiporo beki Michael kwa kuwa hakupata muda wa
kufika mbele ya kamati hiyo kutoa utetezi.
Nyosso ametupwa jela ya kukosa mechi nane za ligi kuu ya Bara kutokana
na kufanya vitendo vya udhalilishaji dhidi ya mshambuliaji Elias Maguli
wa Simba SC wakati wa mechi yao ya raundi ya 10 ya ligi kuu ya Bara
ambayo City ilishinda 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini hapa Januari 28.
Morris, beki wa kati mwenye magoli mawili ligi kuu msimu huu hadi sasa,
ametupwa jela ya kukosa mechi tatu baada ya kubainika alimpiga makusudi
kiwiko shingoni kiungo mshambualiji Mganda Emmanuel Okwi ambaye baada ya
tukio hilo alianguka na kupoteza fahamu kwa dakika tano katika mechi
yao ya raundi ya 12 ya ligi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa Januari 25.
Kamati ya Nidhamu ya TFF iliyoketi chini ya uongozi wa Makamu
Mwenyekiti, Jerome Msemwa imesikiliza utetezi wa beki Michael leo na
kuamua kumtupa jela ya kukosa mechi tatu kwa kuzingatia Ibara ya 48(b)
cha Kanuni za Nidhamu za TFF toleo la 2012.
Masau Bwire, msemaji wa Ruvu Shooting amethibitisha kutolewa kwa adhabu
hiyo dhidi ya mchezaji wao huyo akisema: "Tunaiamini Kamati ya Nidhamu
ya TFF maana ina watu makini na wenye taaluma zao kuhusu masuala ya
sheria."
"Tuna wachezaji wengi, wataziba pengo la Michael. Kamati imeangalia
kanuni za nidhamu zinasemaje na imetend haki kwa kuusikiliza upande wa
mchezaji baada ya wiki iliyopita kumuweka kiporo maana tayari alikuwa
ameshaanza safari ya kuelekea Mbeya wakati anapokea barua ya kuitwa
mbele ya kamati hiyo," ameongeza Bwire.
Matukio yote matatu yaliyowatia hatiani Nyosso, Morris na Michael
hayakuonwa na marefa wa mechi husika. TFF imechukua hatua ya kuwaadhibu
watatu hao baada ya matukio hayo kuripotiwa na vyombo vya habari huku
klabu za Simba na Yanga zikitumia ushahidi wa picha za mnato na video za
vyombo vya habari kuishinikiza TFF kuchukua hatua.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni