Shirikisho la
Mpira wa Miguu nchini (TFF) jana limefanya Mkutano Mkuu wa Mwaka katika ukumbi
wa Morogoro hoteli ya mjini Morogoro ambapo mgeni Rasmi alikua ni mkuu wa mkoa
wa Morogoro Dr Rajabu Rutengwe.
Katika hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano huo, Dr Rutengwe
aliushukuru uongozi wa TFF nchini kwa kuweza kuandaa mkutano mkuu mzuri na wa
kisasa ambao pia ulifanyikia katika mkoa wake wa Morogoro.
Akiongea na wajumbe wa mkutano mkuu Dr Rutengwe alisema, TFF
ina changamoto ambazo inapaswa kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na wadau wa
mpira wa miguu nchini kwa ujumla, changamoto hizo ni kukosekana kwa wataalamu
wa vyakula, wataalamu wa tiba na wataalamu wa saikolojia.
Dr Rutengwe aliomba TFF kwa kushirikiana na serikali
inapaswa kuandaa wataalamu wengi wa masuala hayo ili kuweza kuendana na
mahitaji ya kuwaanda wanamichezo bora ambao watakua tayari kwa ushindani na sio
ushiriki.
Aidha mkuu wa mkoa huyo aliipongeza Kamati ya Utendaji ya
TFF kwa kuupa mkoa wa Morogoro uenyeji wa mkutano mkuu ambapo pia umefanyika
na malengo kufanikiwa kwa asilimia mia
moja, na kusema kwa niaba ya serikali ya mkoa wapo tayari kupokea tena mwaliko
wa uenyeji wa mikutano mbalimbali ya TFF.
Mkutano ulijadili Ajenda za kawaida ambazo ni Kufungua Mkutano ni
Uhakiki wa Wajumbe, Kuthibitisha
Muhtsari wa Mkutano Mkuu uliopita, Yatokanayo na Mkutano uliopita, Hotuba ya
Rais, ripoti kutoka kwa Wanachama, Kuthibitisha
ripoti ya utekelezaji wa Kamati ya Utendaji.
Zingine ni Kuthibitisha
ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu 2013, Kuthibitisha ripoti ya Kamati ya Ukaguzi wa
Hesabu, Kupitisha bajeti ya 2015, Marekebisho ya Katiba, Mengineyo na
Kufunga Mkutano.
Kwa mara ya kwanza
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF limepata bendera yake ambayo
ilipitishwa na mkutano mkuu na asubuhi ya jumapili Machi 15 mwaka huu,
imepandishwa kwa mara ya kwanza Morogoro hoteli.
Aidha wajumbe wa
mkutano mkuu pia wamepitisha azimio la kuanzishwa kwa mfuko wa maendeleo ya
mpira wa miguu nchini (FDF), ambapo kutaundwa kamisheni maalum
itakayoshugulikia suala hilo.
Lengo la kamisheni
hiyo ni kuisaidia TFF kuandaa na kuratibu mipango ya maendeleo ya soka la
watoto, vijana, wanawake nchini na kuviwezesha vyama vya soka vya mikoa (FA),
vyama shiriki vya TFF kujiendesha katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya
soka la vijana.
Pia mkutano mkuu
huo ulitoa azimio la kuitaka serikali itoe msamaha wa kodi kwa vifaa vya
michezo hasa vinavyotumika kufundishia watoto michezo.
Mkutano huo
ulihudhuriwa na wajumbe 125 na kati yao wajumbe watano ni wanawake.
Kikao kijacho cha
mkutano mkuu kitafanyika kati ya mwezi Novemba na Disemba mwaka huu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni